18 Septemba 2021 - 12:11
Jumuiya ya ECOWAS: Alpha Conde Rais aliyepinduliwa wa Guinea yuko katika hali nzuri

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika(ECOWAS) imetangaza kuwa,rais aliyepinduliwa wa Guinea, Alpha Conde, na ambaye amewekwa kizuizini tangu mapinduzi dhidi yake mapema mwezi huu yuko katika hali nzuri.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Taarifa ya ECOWAS imeeleza kuwa, ujumbe wake umefanikiwa kumuona Conde, mjini Conakry, akiwa katika kizuizi cha nyumbani katika hoteli moja ya kifahari.

Hiyo ni taarifa ya kwanza kabisa huru kuhusu hali ya Alpha Conde, tangu kupinduliwa kwake mwanzoni mwa mwezi huu wa Septemba. Ujumbe wa ECOWAS ambao unawajumuisha Rais wa Ghana Nana Akufo Addo, Rais wa Ivory Coast Alassane Outtara, vilevile umekutana na kiongozi wa kijeshi, Mamady Doumbouya.

Taarifa zinasema kuuwa, mazungumzo yao yalikuwa ya wazi na kirafiki, na kwamba wana imani ya kupatikana ufumbuzi wa mgogoro wa sasa wa Guinea. Hayo yanjiri siku moja tu baada ya mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika , ECOWAS, kuchukua hatua ya kuwawekea vikwazo viongozi wa mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa nchini Guinea.

Mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea yameendelea kulaaniwa kieneo na kimataifa huku kukitolewa miito ya kuachiliwa huru Rais Alpha Conde anayeshikiliwa kizuizini na wanajeshi waliofanya mapinduzi.

Wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Guinea wameahidi kuunda serikali ya umoja wa kitaifa itakayoongoza kipindi cha mpito kuelekea demokrasia, lakini bila kutaja muda wa serikali hiyo.

342/